Friday, February 10, 2012

Mkia

KATIKA demokrasia, serikali ni mkia,
Nyati ni wao raia, kwayo wanayoamua,
Hukua yanayokuwa, wapewe wanaopewa,
Mkia hautingishi,
Katika hii arshi!
Nyati hutingisha mkia,
Mkia nyati haumwezi!

Hautingishi mkia, nyati akanyong'onyea
Ila yeye ndiye mjua, kuutikisa mkia,
Serikali ilokuwa, ikawa au kutokuwa,
Mkia hautingishi,
Katika hii arshi!
Nyati hutingisha mkia,
Mkia nyati haumwezi!

Ila huweza tokea, wababe wakaamua,
Waliokuwa mkia, nyati kumchokoroa,
Na pale alipotulia, hasira ikamjia,
Mkia hautingishi,
Katika hii arshi!
Nyati hutingisha mkia,
Mkia nyati haumwezi!

Tope anayechezea, thamani akatolewa,
Mjinga akadhaniwa, hajui ya kuyajua,
Njaa na yake tamaa, vibaya ikatumiwa,
Mkia hautingishi,
Katika hii arshi!
Nyati hutingisha mkia,
Mkia nyati haumwezi!

Mengi uhaidiwa, yasiwe na kutimia,
Miaka ikajongea, pale pale kubakia,
Ikawa kuendelea, kwake kama ruia,
Mkia hautingishi,
Katika hii arshi!
Nyati hutingisha mkia,
Mkia nyati haumwezi!

Huvimbisha zake pua, kwa jazba kupumua,
Pembe akazinyanyua, na miguu kuibua,
Topeni akajizoa, juujuu akapaa,
Mkia hautingishi,
Katika hii arshi!
Nyati hutingisha mkia,
Mkia nyati haumwezi!

Chini hatorudia, hadi pembe zimeua,
Damu akaisikia, puani kaipumua,
Ndipo hapo hutulia, akajua lakujua,
Mkia hautingishi,
Katika hii arshi!
Nyati hutingisha mkia,
Mkia nyati haumwezi!

Nyati wanaomchezea,balaa wajitakia,
Mapema nawaambia, ya maana kuamua,
Patashika itakua, pasiwe cha kubakia,
Mkia hautingishi,
Katika hii arshi!
Nyati hutingisha mkia,
Mkia nyati haumwezi!

Juu mliokaa, bila kuwa manufaa,
Mkanona na kubwia, na ujinga kuzidia,
Nakama ikiingia, hakuna cha mswalia,
Mkia hautingishi,
Katika hii arshi!
Nyati hutingisha mkia,
Mkia nyati haumwezi!

Nyati hataki dunia, ila topeni kukaa,
Majani yakichanua, chakula chake hujaa,
Na wanae akizaa, hujaa yake maziwa,
Mkia hautingishi,
Katika hii arshi!
Nyati hutingisha mkia,
Mkia nyati haumwezi!

Mambo mkijifanyia, topeni kumuondoa,
Na majani kutosia, nyie viguu na njia,
Nyati atapozidiwa, zahama ataizua,
Mkia hautingishi,
Katika hii arshi!
Nyati hutingisha mkia,
Mkia nyati haumwezi!

Nyie mliozoea, unyati kuutumia,
Bila ya kujitambua, si zaidi ya mkia,
Hili msipoangalia, mabaya mwajitakia,
Mkia hautingishi,
Katika hii arshi!
Nyati hutingisha mkia,
Mkia nyati haumwezi!

Kila kitu wachukia, hazina kuifagia,
Wananchi wakaishiwa, na ufakiri kukua,
Watu wakaongezewa, adha, dhiki na njaa,
Mkia hautingishi,
Katika hii arshi!
Nyati hutingisha mkia,
Mkia nyati haumwezi!

Wanaousaidia, ukatingisha mkia,
Akili wasiotumia, kusagwa kama ngamia,
Ni balaa twaiea, lazima kujaing'oa,
Mkia hautingishi,
Katika hii arshi!
Nyati hutingisha mkia,
Mkia nyati haumwezi!

Siku kuwahesabia, hesabu wasiojua,
Wakati ukiwadia, zawadi yao kupewa,
Ndivyo itakavyokuwa, vinginevyo haitakuwa,
Mkia hautingishi,
Katika hii arshi!
Nyati hutingisha mkia,
Mkia nyati haumwezi!

Watu macho wafungua, haki zao kuzijua,
Hukumu wataitoa, wakati ukiwadia,
Wanafiki walokuwa, lazima kusimbuliwa,
Mkia hautingishi,
Katika hii arshi!
Nyati hutingisha mkia,
Mkia nyati haumwezi!

No comments: