Friday, February 10, 2012

Gazeti la chama jaa

Uongo linavyojaa, hakika hii balaa,
Huzua wanayozua, na umbeya kuutia,
Hakuna la kuzingatia, uchama tupu lajaa,
Gazeti la chama jaa, hasara ukinunua!

Linachangia kuua, haki pia na usawa,
Wakubwa lawatetea, hata watu wakiuua,
Tumeona Tunisia, twangojea Tanzania,
Gazeti la chama jaa, hasara ukinunua!

Mamluki huchukua, uandishi kuachiwa,
Na kada mtarajiwa, mhariri anakuwa,
Kazi yao ni umbeya, na ukweli kukataaa,
Gazeti la chama jaa, hasara ukinunua!

Huwa kama changudoa, jinsi wanavyotumia,
Haya huwakimbia, na aibu kuwaambaa,
Wanenalo ni nazaa, si watu wa kusikiwa,
Gazeti la chama jaa, hasara ukinunua!

Maneno wanavyojua, kuunda na kutumia,
Uongo yaliyojaa, akili hukupindua,
Anzali kama ukiwa, rahisi kuzainiwa,
Gazeti la chama jaa, hasara ukinunua!

Na wanademokrasia, watu hawa wawajua,
Watawaliwa na njaa, umalaya kuridhia,
Hukumu yawangojea, kiyama kikiingia,

Unafiki wamejaa, wakafikia kuua,
Watu kuwasingizia, hata wasiyotambua,
Kupatiliza yafaa, na laana kuwaombea,
Gazeti la chama jaa, hasara ukinunua!

Yarabi nakulilia, jehanamu kuambaa,
Vigogo kutonitumia, ukweli nikachuuzia,
Kalamu niliyopewa, uongo kutoridhia,
Gazeti la chama jaa, hasara ukilinunu!

No comments: