BATI waweza kutia, uwanja ukaanua,
Mipaka ukaitia, kujenga wadhamiria,
Ila hili majaliwa, hata ukitia nia,
Mtu kuweka msingi, si hakika ya kujenga!
Ujenzi ni majaliwa, na mtu kuandikiwa,
Msingi wanaoitia, hadi wakamalizia,
Ni wachache walokuwa, wengi wao hupwelea,
Mtu kuweka msingi, si hakika ya kujenga!
Hushidnwa kuendelea, katikati kuishia,
Bado ipo yao nia, ila uwezo wapwaya,
Mahitaji yazidia, kuliko kinachoingia,
Mtu kuweka msingi, si hakika ya kujenga!
Na hili jema kujua, mtu unapojaliwa,
Muumba ukamjua, na dhamira kumwachia,
Hubariki yalokuwa, hadi yaje kutimia,
Mtu kuweka msingi, si hakika ya kujenga!
Msingi ukanyanyua, imara uliokuwa,
Kisha kuta ukatia, na lenta kuimwagia,
Na boriti kufungia, paa ukalipaua,
Mtu kuweka msingi, si hakika ya kujenga!
Milango ukafungia, madirisha nayo pia,
Fenicha ukazitia, makabati yalokuwa,
Na vyumba kujipmbia, kadri unavyojua,
Mtu kuweka msingi, si hakika ya kujenga!
Neru ukamiminia, na kumwaiya chokaa,
Na rangi kuziwania, zote zinazovutia,
Nje ukamalizia, na bustani kukua,
Mtu kuweka msingi, si hakika ya kujenga!
Ukuta kuzungushia, ulinzi ukiamua,
Na kuondoa udhia, jirani waliokuwa,
Na geti kujiwekea, tena la kujifungua,
Mtu kuweka msingi, si hakika ya kujenga!
Na kengele ukatia, hodi ukazikataa,
Na taa kumulikiwa, hata usiku ukiwa,
Na ving'ora vikajaa, wevi wapate kimbia,
Mtu kuweka msingi, si hakika ya kujenga!
Siku ikajafikia, ya wewe kujahamia,
Ziraili akatua, na roho kuichukua,
Wengine wataingia, wewe hautaingia,
Mtu kuweka msingi, si hakika ya kujenga!
Yako haiwezi kuwa, huwa ya atayenunua,
Au mrithi akiwa, ataka kuitumia,
Wewe kwana kuhamia, ulikoishandaliwa,
Mtu kuweka msingi, si hakika ya kujenga!
Friday, February 17, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment