Monday, February 6, 2012

Uheshimiwa kanisani?

Ya msikiti si yenu, wakubwa mliokuwa,
Hapa si pahali penu, si siasa ni daawa,
Zichukueni fununu, kwingine kuhamishia,
Uheshimiwa kanisani,
Hivi Mungu twamchezaea?

Kanuni tunazijua, ibada yake sheria,
Wa kwanza kutangulai,safu mbele akakaa,
Nyuma wanaoingia, lazima nyuma kukaa,
Uheshimiwa kanisani,
Hivi Mungu twamchezaea?

Dini mnatangazia, siasa haitofaa,
Mseti kujipikia, chakula kibichi huwa,
Nasi tunawambia,sera zenu si dua,
Uheshimiwa kanisani,
Hivi Mungu twamchezaea?

Protokoli ya dua, na ibada twaijua,
Ya siasa ilokuwa, kwingine kuitumia,
Heshima wa kwanza kuwa, wengine wakafuatia,
Uheshimiwa kanisani,
Hivi Mungu twamchezaea?

Nani anayemjua, mtukufu alokuwa,
Aliyekwishachaguliwa, na pepo keshaipewa,
Yumkini hatokuwa, mkubwa tunayemjua,
Uheshimiwa kanisani,
Hivi Mungu twamchezaea?

Huyo aweza akawa, mbaya anayechukiwa,
Mbingu zimemkataa, kwa dhambi anazochukua,
Hasira mkaivaa, baa kuvurumishiwa,
Uheshimiwa kanisani,
Hivi Mungu twamchezaea?

Na uchafu ulokua, patakatifu kukaa,
Malaika wakapaa, na nje kuondokea,
Uoza kuukataa, hewa unavyochafua,
Uheshimiwa kanisani,
Hivi Mungu twamchezaea?

Viongozi mwatakiwa, haya kuyafafanua,
Msije mkaichezea, nyumba ya Mungu ilokuwa,
Kwa kutaka jinyanyua, migongoni kupitia,
Uheshimiwa kanisani,
Hivi Mungu twamchezaea?

Ukubwa mkiwania, hapa si pa kujipatia,
Nendeni kunakofaa, ya kwenu kuhangaikia,
Waumini twakataa, si ibadani yakawa,
Uheshimiwa kanisani,
Hivi Mungu twamchezaea?

Februari 8. 2012,
Dar es Salaam.

No comments: