Mimi mja wako dhaifu
Nasujudu mbele yako mtukufu
Kwa unyenyekevu na hofu
Ninakusihi Raufu
Kunizawadia Afu
Afueni na nafuu.
Miimi niliye dhalili
Ni dhoofu yangu hali
Ila kwa amri yako Aali
Hukinusuru kiwiliwili
Na kuzinoa zangu akili
Kiisha kwa kupata siha
Nifanze unayonituma:
Sina ninalolijua
Ila yale uliyonifunulia
Kadiri iliyokuwa
Ni yako niliyopewa
Na cheo nilichopewa,
Si ukubwa ila kutumikia
Naomba macho kunifungua
Lililo sahihi kuling'amua!
Mali niliyoshikilia,
Si yangu iliyokuwa
Ni wewe ulonigawia
Kwa muda kushikilia
Ili niwe ninawapatia
Uliokwishawachagua
Ni bomba nafusi imekua
Vya wengine kupitishia
Na hili nimeridhia
Naahidi kukutumikia.
Cheo wala mali visinibadili
Kwako mimi bado ni dhalili,
Nipe angavu na fasili akili
Hili daima kulitambua.
Iwe kwa kila iwavyo hali
Hulka yangu iwe kamili
Niache kuiga kama tumbili
Tamaduni za nisiowajua!
Nisetiti kwa mapungufu yangu
Nisamehe pia na dhambi zangu
Nionyeshe njia kupita ifaayo
Shetani kusiko wake wayo
Ni yako njia hiyo iliyonyooka
Na wapitao ndiwe unayewachagua
Naomba na mimi kunichagua
Niwe ni mmoja kati yao
Nisiwe kati ya wale uliokwisha waghadhabikia!
Februari 6, 2012
Dar es Salaam.
Monday, February 6, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment