Monday, February 13, 2012

Usafi unaotakiwa

Michafu yetu mitaa, kila mtu atambua,
Hatujaijenga tabia, usafi kuuridhia,
Japo majuu twapaa, ugenini kujionea,
Usafi tunaotaka, si tu wa barabarani,
Bali pia ni wa ndani,
na hususani rohoni,
au ikawa moyoni!

Hata ikulu ikiwa, ukienda chungulia,
Uchafu utagundua, pembeni umesogea,
Miji mingi ni balaa, inshakuwa kinyaa,
Usafi tunaotaka, si tu wa barabarani,
Bali pia ni wa ndani,
na hususani rohoni,
au ikawa moyoni!

Tuanouzungumzia, wazidi huu wa mtaa,
Ni tulivyoichafua, mioyo tuliyopewa,
Machafu twafirikia,wa chini na wa juu pia,
Usafi tunaotaka, si tu wa barabarani,
Bali pia ni wa ndani,
na hususani rohoni,
au ikawa moyoni!

Ama ni uongo kutia, uzaini na hadaa,
Kauli tunatoa, ukweli umelaniwa,
Na simu twazitumia, madhambi kuongezea,
Usafi tunaotaka, si tu wa barabarani,
Bali pia ni wa ndani,
na hususani rohoni,
au ikawa moyoni!

Wanasiasa wazua, mengi yasiyotufaa,
Na uongo kutumia, wajinga tukadhaniwa,
Leo sisi twatumiwa, badala ya kuwatumia,
Usafi tunaotaka, si tu wa barabarani,
Bali pia ni wa ndani,
na hususani rohoni,
au ikawa moyoni!

Wezi tumekwishakua, wenyewe twajiibia
Hazina twaichimbua, wakubwa kujigawiwa,
Masikini walokuwa, ardhi tupu waachiwa,
Usafi tunaotaka, si tu wa barabarani,
Bali pia ni wa ndani,
na hususani rohoni,
au ikawa moyoni!

Malaya tumeshakua, twauza na kununua,
Zimetukimbia haya, aibu imetuishia,
Na laana inatujia, huku twaiangalia,
Usafi tunaotaka, si tu wa barabarani,
Bali pia ni wa ndani,
na hususani rohoni,
au ikawa moyoni!

Unafiki unakua, kwa tunayoyaonge,
Uzushi twajifanyia, na maradhi twauguwa,
Twazidi jishindilia, kule kusikotufaa,
Usafi tunaotaka, si tu wa barabarani,
Bali pia ni wa ndani,
na hususani rohoni,
au ikawa moyoni!

Televisheni nazaa, vibaya twazitumia,
Uongo kutangazia, na ukweli kuzuia,
Mola atuangalia, na moto watungojea,
Usafi tunaotaka, si tu wa barabarani,
Bali pia ni wa ndani,
na hususani rohoni,
au ikawa moyoni!
Usafi tunaotaka, si tu wa barabarani,
Bali pia ni wa ndani,
na hususani rohoni,
au ikawa moyoni!

Hata dini walokuwa, viongozi watumiwa,
Uongo wanaugawa, kama pipi wadhania,
Upako wakipakua, hakuna kinachobakia,
Usafi tunaotaka, si tu wa barabarani,
Bali pia ni wa ndani,
na hususani rohoni,
au ikawa moyoni!

Haki twajiuzia, na wengine kununua,
Baraka twazikimbia, nuksi twajitakia,
Na kila ukichungua, viongozi wajijua,
Usafi tunaotaka, si tu wa barabarani,
Bali pia ni wa ndani,
na hususani rohoni,
au ikawa moyoni!

Nani amewaambia, uongozi budi kuwa,
Kwa uongo kutumia, na hadaa kutumia,
Hayo mnayojipalilia, hivi kweli mwayajua?
Usafi tunaotaka, si tu wa barabarani,
Bali pia ni wa ndani,
na hususani rohoni,
au ikawa moyoni!

Magazeti yatumiwa, kama vile ni malaya,
Uongo kushangilia, na ukweli kuzomea,
Hili latia kinyaa, linavyoendelea,
Usafi tunaotaka, si tu wa barabarani,
Bali pia ni wa ndani,
na hususani rohoni,
au ikawa moyoni!

Mihimili yatakiwa, kipato kufanania,
Waandishi walokuwa, na wanasiasa pia,
Watumishi kuwa sawa, polisi kutotumiwa,
Usafi tunaotaka, si tu wa barabarani,
Bali pia ni wa ndani,
na hususani rohoni,
au ikawa moyoni!

Mmoja akizidishiwa, wengine atatumia,
Kuwanonga kuridhia, au maguvu kutumia,
Mbaka ninaiachia, wote kuja kulaniwa,
Usafi tunaotaka, si tu wa barabarani,
Bali pia ni wa ndani,
na hususani rohoni,
au ikawa moyoni!

Nchi ninailia, mwendo imekosea,
Ujuaji inajitia, kumbe inajiumbua,
Karibu waliokuwa, indiketa watuwashia,
Usafi tunaotaka, si tu wa barabarani,
Bali pia ni wa ndani,
na hususani rohoni,
au ikawa moyoni!

Pasipo wasafi kuwa, mengi tutayatengua,
Nchi ije kulemaa, tushindwe hata tembea,
Na hapo tukifikia, wengi wataathiriwa,
Usafi tunaotaka, si tu wa barabarani,
Bali pia ni wa ndani,
na hususani rohoni,
au ikawa moyoni!

Lazima kujichungua, na wenyewe kujijua,
Nini nchi kuifanyia, na watu kuendelea,
Sio tu kuvitumia, wazalishavyo raia,
Usafi tunaotaka, si tu wa barabarani,
Bali pia ni wa ndani,
na hususani rohoni,
au ikawa moyoni!

Panahitajika nia, nia ya kuendelea,
Na watu kweli kutoa, shidani walimokuwa,
Ufakiri kupotea, na neema kuingia,
Usafi tunaotaka, si tu wa barabarani,
Bali pia ni wa ndani,
na hususani rohoni,
au ikawa moyoni!

Pasipo wasafi kuwa, pamoja na vyama pia,
Hili hatulifikia, wala kuja kujaliwa,
Nyikani tutapotea, jangwani kwenda ishia,
Usafi tunaotaka, si tu wa barabarani,
Bali pia ni wa ndani,
na hususani rohoni,
au ikawa moyoni!

Yarabi twakulilia, tupe wanaotufaa,
Viongzi Tanzania, kazi wanaoijua,
Umaskini kutoa, na nchi kutochezewa,
Usafi tunaotaka, si tu wa barabarani,
Bali pia ni wa ndani,
na hususani rohoni,
au ikawa moyoni!

Nafuu tukaijua, kama hai kupumua,
Sio wafu tulokuwa, tunangoja kufukiwa,
Azizi unayajua, na wabaya unawajua,
Usafi tunaotaka, si tu wa barabarani,
Bali pia ni wa ndani,
na hususani rohoni,
au ikawa moyoni!

No comments: