Nani aliyewatuma, au kisasi mwatukua,
Nahisi kuna nakama, hawajui wasojua,
Unapojenga chuki, kwa polisi na raia:
Taifa unaliua,
Umoja unaambaa,
Na amani yapotea!
Zana mnazozifuma, vitani zilitakiwa,
Au migodi kuchuma, hicho kinachoibiwa,
Sio kuutesa umma, na uyatima kwingia,
Unapojenga chuki, kwa polisi na raia:
Taifa unaliua,
Umoja unaambaa,
Na amani yapotea!
Mwaturudisha nyuma, juu mliotangulia,
Na busara na hekima, yawa kama isokuwa,
Ni mashaka na tuhuma, nyuma yanawafatia,
Unapojenga chuki, kwa polisi na raia:
Taifa unaliua,
Umoja unaambaa,
Na amani yapotea!
Mambo yataka kalima, si magomvi kuyazua,
Utu usio heshima, haikubali dunia,
Hata mtumie vyuma, haki itapiganiwa,
Unapojenga chuki, kwa polisi na raia:
Taifa unaliua,
Umoja unaambaa,
Na amani yapotea!
Mwatia watu ulema, ndani waliotulia,
Na uongo kuusema, deraya wanavamia,
Hachagui la kusema, muongo alolaaniwa,
Unapojenga chuki, kwa polisi na raia:
Taifa unaliua,
Umoja unaambaa,
Na amani yapotea!
Nchi yataka adhama, watu waliojaliwa,
Wenye kuwa roho njema, na uhai kuulea,
Si wenye kuwasakama, hatia wasiokuwa,
Unapojenga chuki, kwa polisi na raia:
Taifa unaliua,
Umoja unaambaa,
Na amani yapotea!
Mkoloni anasema, mbinu zetumia,
Dhidi ya kwao umma, kama tulivyoanzia,
Ni ipi yao heshima, kulikoni tulokuwa?
Unapojenga chuki, kwa polisi na raia:
Taifa unaliua,
Umoja unaambaa,
Na amani yapotea!
Weupe watusakama, weusi wameingia,
Feli na zao kalima, yale yale yamekuwa,
Dunia hii sinema, na mcheza utamjua!
Unapojenga chuki, kwa polisi na raia:
Taifa unaliua,
Umoja unaambaa,
Na amani yapotea!
Mola wetu muadhama, tabia aichukia,
Na wasio na hekima, kwenu kujipalilia,
Wakidai mwendo nyuma, bei
Unapojenga chuki, kwa polisi na raia:
Taifa unaliua,
Umoja unaambaa,
Na amani yapotea!
No comments:
Post a Comment