Wengine nawashangaa, lawama wanazotoa,
Laiti wangelijua, hili wangelifukia,
Siye tumeandikiwa, nyie bado andikiwa,
Sisi twatibiwa nje, hospitali za Uswazi:
Zatuhusu kitu gani?
Wa kushoto na kulia, India tunaingia,
Au Sauzi kuridhia, Wazulu kuwaamkua,
Nyie hamjafikia, walal hamtafikia,
Sisi twatibiwa nje, hospitali za Uswazi:
Zinatuhusu kitu gani?
Wa chini haitokuwa, juu akaruhusiwa,
Na juu hukataliwa, aende chini kukaa,
Hii ni kweli ya dunia, hata pepo yatambua,
Sisi twatibiwa nje, hospitali za Uswazi:
Zinatuhusu kitu gani?
Msije mkajitia, kwa msiyo yaelewa,
Vibaya mtaumia, na mengi mkazushiwa,
Na za wakubwa dawa, kwenu sumu zitakuwa,
Sisi twatibiwa nje, hospitali za Uswazi:
Zinatuhusu kitu gani?
Usawa hautokuwa, katika hii dunia,
Angalia pepo pia, wa peponi huingia,
Kahaliika nao pia, wa motoni wakubaliwa,
Sisi twatibiwa nje, hospitali za Uswazi:
Zinatuhusu kitu gani?
Mila zetu zakataa, vingine ni kujikwaa,
Maisha ni kuchagua, chagua kuendelea,
Kuiga hakutokufaa, kwani waweza lemaa,
Sisi twatibiwa nje, hospitali za Uswazi:
Zinatuhusu kitu gani?
Februari 8, 2012,
Dar es Salaam.
Monday, February 6, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment