Kuna sheria na unaa, ukweli nayo hadaa,
Uhai ninavyojua, juu ya kila kitu huwa,
Vinginevyo haijawa, wala sijawaelewa,
Jambo hili zito sana, kwa hiyo lisizungumzwe ?
Jambo zito kutokea, watu hushughulikia,
Hawawezi liachia, eti kesho kungojea,
Tulikwishaambiwa, ngoja ngoja ni adawa,
Jambo hili zito sana, kwa hiyo lisizungumzwe ?
Ngojangoja ni adawa, matumbo yataumia,
Leo linalotakiwa, kesho kutokungojea,
Bila kuyazungumzia, uzito huongezea,
Jambo hili zito sana, kwa hiyo lisizungumzwe!
Akili tunatambua, kila mtu kajaliwa,
Mme akitokea, ushauri kukataa,
Akajifanya ajua, mke kutomsikia, J
ambo hili zito sana, kwa hiyo lisizungumzwe!
Akajifanya ajua, mke kutomsikia,
Mwenyewe akaamua, kinyume ilivyokuwa,
Ikitokea balaa, nani atamlilia?
Jambo hili zito sana, kwa hiyo lisizungumzwe!
Binadamu atakiwa, ushauri kupokea,
Wengi vikao kukaa, mawazo wakayatoa,
Na wale wanaoamua, mengine yakawafaa,
Jambo hili zito sana, kwa hiyo lisizungumzwe!
Bunge ninalishangaa, protokoli kujikwaa,
Wakashindwa kuelewa, uhai hautongojea,
Wanaipinda sheria, kwa uhai juu kuwa,
Jambo hili zito sana, kwa hiyo lisizungumzwe
Uchama unaugua, na nchi yateketea,
Na huu tukiuachia, pabaya tutaingia,
Nyie mnaosinzia, amkeni twawaambia,
Jambo hili zito sana, kwa hiyo lisizungumzwe!
Wananchi wanaugua, vikao vyaendelea?
Wazazi wajifungua, hatihati kutokea,
Mara moja kuamua, ndilo linalotakiwa,
Jambo hili zito sana, kwa hiyo lisizungumzwe!
Mahali hujafikia, huruma ikapotea,
Viongozi kutojua, keki yetu kuigawa,
Wao kubwa kuchukua, kidunchu wakaachia,
Jambo hili zito sana, kwa hiyo lisizungumzwe!
Uislamu wanambia, mizani kuitumia,
Kiapo batili huwa, haki inapopungua,
Huku tunajionea, walao si wa kuzaa,
Jambo hili zito sana, kwa hiyo lisizungumzwe!
Karne imefikia, viongozi kutambua,
Wanatakiwa raia, juu kwanza wao kuwa,
Kisha mkiendelea, na wao wakajifaa,
Jambo hili zito sana, kwa hiyo lisizungumzwe!
Uongozi kuutwaa, na hazina kubomoa,
Yote wakayachukua, watu wanayakataa,
Sasa nchi mbele kuwa, ndilo linaloazimiwa,
Chozi la mamba ukiwa, hakuna wa kusikia,
Hayo mliyozoea, lazima kuyaachia,
Nyakati zajifungua, mengi budi kufumua,
Jambo hili zito sana, kwa hiyo lisizungumzwe!
Februari 7, 2012,
Dar es Salaam
Saturday, February 11, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment