Monday, February 6, 2012

Maiti walio hai

Maiti walio hai, wa leo Watanzania,
Usidanie nishai, haya ninayokwambia,
Ni ukweli ukinai, ufukara unaua,
Mafuta ya taa roho, na umeme ndio moyo,
kuni na makaa nayo, mambo ni hayohayo,
Hivi ukinyofolewa,
Maiti unabakia!
Damu ikichukuliwa,
Umemaliza raia!

Chakula sasa papai,shilingi ilobakia,
Inaadimika chai, anasa imeshakua,
Ipi ilo njema rai, yaweza kusaidia?
Mafuta ya taa roho, na umeme ndio moyo,
kuni na makaa nayo, mambo ni hayohayo,
Hivi ukinyofolewa,
Maiti unabakia!
Damu ikichukuliwa,

Siasa hazitufai, uchumi zinazoua,
Na viongozi karai, nchi wanaipindua,
Kichwa chini huzirai, gizani kuning'inia,
Mafuta ya taa roho, na umeme ndio moyo,
kuni na makaa nayo, mambo ni hayohayo,
Hivi ukinyofolewa,
Maiti unabakia!
Damu ikichukuliwa,
Umemaliza raia!

Vipi mwapandisha bei, na uhai kuchezea,
Ya wapi yenu digrii, uchumi mlosomea,
Haifai hali hii, kwengine mngezolewa,
Mafuta ya taa roho, na umeme ndio moyo,
kuni na makaa nayo, mambo ni hayohayo,
Hivi ukinyofolewa,
Maiti unabakia!
Damu ikichukuliwa,
Umemaliza raia!

Maiti tungali hai, kwa kuwa tunapumua,
Nafusi zimekinai, kwa nchi kusinyaa,
Huku watu wajidai, eti tunaendelea,
Mafuta ya taa roho, na umeme ndio moyo,
kuni na makaa nayo, mambo ni hayohayo,
Hivi ukinyofolewa,
Maiti unabakia!
Damu ikichukuliwa,
Umemaliza raia!

Unafiki haufai, dini zote zakataa,
Ukweli ukikinai, thamani hukupotea,
Ukawa mtu hufai, watu kitu kuwaambia,
Mafuta ya taa roho, na umeme ndio moyo,
kuni na makaa nayo, mambo ni hayohayo,
Hivi ukinyofolewa,
Maiti unabakia!
Damu ikichukuliwa,
Umemaliza raia!
Umemaliza raia!

Februari 6, 2012
Dar es Salaam.

No comments: