Soko halijajaliwa, na mwenyewe naye kuwa,
Hupokea, huachia, kila kiachoingia,
Na mtaka kuchukua, kumiliki haijawa,
Hujiondoa sokoni, anayechezea soko!
Kula anayechezea, wasaa humuachia,
Hulala na kudhania, tajiri ameshakuwa,
Ila akistukia, soko linamzomea,
Hujiondoa sokoni, anayechezea soko!
Soko ni kama kichaa, urafiki haujawa,
Halina wa kumjua, wala wa kumwabudia,
Hufanza linaloamua, silo unaloamua,
Hujiondoa sokoni, anayechezea soko!
Utashi ukijitia, waja kweli kufulia,
Huja likakukataa, mbali kukufukuzia,
Ukadhani wataniwa, kumbe kweli yamekuwa,
Hujiondoa sokoni, anayechezea soko!
Akili mali tambua, kila mtu kajaliwa,
Za soki zimezidia, ni mtaji ulokuwa,
Hutenda na kutendua, bila wewe kukujua,
Hujiondoa sokoni, anayechezea soko!
Kushauri inafaa, kabla haujaamua,
Wapo wanaolijua, kuliko unayolijua,
Hawa ukiwasikia, shari utazikimbia,
Hujiondoa sokoni, anayechezea soko!
Mjanja hujanjuliwa, mjinga mwerevu kuwa,
Na ndivyo inavyokuwa, katika hii dunia,
Hukaa wasiokaa, wasimame walokaa,
Hujiondoa sokoni, anayechezea soko!
Yangu nimewausia, wasikie wa kusikia,
Kijijini narejea, mpungu kupalilia,
Wali siwezi nunua, bei mjini zapaa,
Hujiondoa sokoni, anayechezea soko!
Monday, February 13, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment