GARI uliowachia, kuendesha wanajua?
Au sukani waachia, frii kujiendea?
Ajali naingojea, siku nyingi haitokuwa,
Kaka yangu nauliza, kwenda nje wapania:
Nyumba wamwachia nani,
Jamaa wako salama?
Basi lako waachia, la wengine wadandia,
Suka ajabu watoa, watu wanakushangaa,
Konda amedandia, kuendesha hajajua,
Kaka yangu nauliza, kwenda nje wapania:
Nyumba wamwachia nani,
Jamaa wako salama?
Mkuu anangojewa, kwenye kiti keshakaa,
Mbona rivasi atia, badala moja kutia,
Bonde nyuma limekaa, na kiama chatujia,
Kaka yangu nauliza, kwenda nje wapania:
Nyumba wamwachia nani,
Jamaa wako salama?
Deiwaka wamejaa, mikoa hadi wilaya,
Kila siku twasikiya, mashimo wanavyoingia,
Kujiamini sanaa, na mafao si kufaa,
Kaka yangu nauliza, kwenda nje wapania:
Nyumba wamwachia nani,
Jamaa wako salama?
Wanashiba wenye njaa, mlo wakishaupewa,
Ila yaja kubakia, wenye njaa watawajua?
Nani wa kujitendea, yeye anayoamua,
Kaka yangu nauliza, kwenda nje wapania:
Nyumba wamwachia nani,
Jamaa wako salama?
Na mkuu wa mkoa, ambaye huteuliwa,
Aweza lea raia, au nguvu atumia,
Fimbo ndogo limekua, sasa gogo kakamia ?
Kaka yangu nauliza, kwenda nje wapania:
Nyumba wamwachia nani,
Jamaa wako salama?
Gari lisilodhibitiwa, liendako hutojua,
Huwa ni
Na ndivyo inavyokuwa, na yote tunayajua,
Kaka yangu nauliza, kwenda nje wapania:
Nyumba wamwachia nani,
Jamaa wako salama?
Gari wakiachiwa, kuendesha wasojua,
Huishiwa abiria, amani ikapotea,
Akabaki kulia, yarabi kumuokoa,
Kaka yangu nauliza, kwenda nje wapania:
Nyumba wamwachia nani,
Jamaa wako salama?
Na mkuu wa wilaya, watu wake awajua,
Au kazi kusakazia, raia wakaratua,
Na vibaka kuingia, hata nje walokuwa,
Kaka yangu nauliza, kwenda nje wapania:
Nyumba wamwachia nani,
Jamaa wako salama?
Kamanda waliopewa, ni kina Mabula pawa,
Au busara wapewa, kihaki kuyaamua,
Na siyo ya kufokewa, na amri za umbeya?
Kaka yangu nauliza, kwenda nje wapania:
Nyumba wamwachia nani,
Jamaa wako salama?
Na waziri
Afanze ya kumfaa, kwa wengine kiama kuwa,
Bila kufuatilia, nchi haitopotea?
Kaka yangu nauliza, kwenda nje wapania:
Nyumba wamwachia nani,
Jamaa wako salama?
Miundo iliyokuwa, watu geti wakataa,
Inapaswa kufungua, uhuru watu wakawa,
La sivyo yatatokea, kwingine yanayotokea,
Kaka yangu nauliza, kwenda nje wapania:
Nyumba wamwachia nani,
Jamaa wako salama?
Mifumo watu wafumua, yawabana kifua,
Na miundo waezua, madirisha kupanua,
Na milango kuitia, mikubwa iliyokuwa,
Kaka yangu nauliza, kwenda nje wapania:
Nyumba wamwachia nani,
Jamaa wako salama?
Wewe ukiendelea, mlangoni kuzuia,
Waktioka wakatua, hapo ulipotegea,
Pembeni watakufagia, mbele wende angukia,
Kaka yangu nauliza, kwenda nje wapania:
Nyumba wamwachia nani,
Jamaa wako salama?
Yanayotokea Mbeya, Arusha nako Songea,
Ujumbe nausikia, nawe haujasikia?
Mikoa huru ikiwa, balaa tutaambaa,
Kaka yangu nauliza, kwenda nje wapania:
Nyumba wamwachia nani,
Jamaa wako salama?
Kuzidi kung'ang'ania, mabaa yakaribia,
Hakuna la kujivua, kwa wingi tutaangamia,
Tunaishindwa mikoa, tutaiweza
Kaka yangu nauliza, kwenda nje wapania:
Nyumba wamwachia nani,
Jamaa wako salama?
No comments:
Post a Comment