Kila mtu ashangaa, dhiki waikimbilia,
Wengi wanavyodhania, pengine umechezewa,
Kulogwa inshakuwa, huu nusu ukichaa,
Starehe gani hii, dhiki kuikimbilia ?
Si bure umechezewa, au mzazi kachukia,
Mema unayotendewa, kwako ubaya inkuwa?
Wengine waililia, nafasi uliyopewa,
Starehe gani hii, dhiki kuikimbilia ?
Uhuru umegaiwa, wewe waudhihakia,
Unaibeza tabia, ya ulua wa kufaa,
Na uchafu wautwaa, mwilini kujimwagiwa,
Starehe gani hii, dhiki kuikimbilia ?
Huu kama ukichaa, naona ilivyokuwa,
Kila siku ikiingia, hali huwa kote mbaya,
Watu wanaulizia, kanyimwa na kupagawa?
Starehe gani hii, dhiki kuikimbilia ?
Wabaya washangilia, zuzu kusesembuliwa,
Raha waitamania, ije kuwaangukia,
Kila wakikazania, kofuli bado yatiwa,
Starehe gani hii, dhiki kuikimbilia ?
Lango langu kufungua, haijawa, nanuia,
Hadi akitokea, malaika atembea,
Urulaini radhia, duniani akajaa,
Starehe gani hii, dhiki kuikimbilia ?
Mazuri wayaachia, mabaya wang'ang'ania,
Nini kinakuzuzua, bado hatujakijua,
Kila pembe twaulizia, majibu hatujapewa,
Starehe gani hii, dhiki kuikimbilia ?
Mtaji umeitwaa, nani kukusaidia,
Wazazi nini kupewa, hali pato umeua?
Wallahi nakusikitia, ninatamani kulia,
Starehe gani hii, dhiki kuikimbilia ?
Raha uliidhania, nje utajiokotea,
Ndani ukapachukia, na wa ndani kuwa udhia,
Laiti ungelijua, ndani ungejiangalia,
Starehe gani hii, dhiki kuikimbilia ?
No comments:
Post a Comment