Monday, February 6, 2012

MNAFIKI

Utu ukiuachia, na vitu kuvamia,
Wapambe hufurahia, kukuchuna kwa ridhaa,
Na wewe ukadhania, maarufu umekua,
Mnafiki hana haya, huvaa yanayompwaya!

Kiumbe huna mabawa, huruki utarukiwa,
Haya ukipapatikia, yale utatindikiwa,
Na juu huwezi kuwa, wote ukawazidia,
Mnafiki hana haya, huvaa yanayompwaya!

Hata rais akiwa, wapo juu walokuwa,
Wengine hujitakia, na wengine hununuliwa,
Ila ukweli chukua, mengine hayana waa,
Mnafiki hana haya, huvaa yanayompwaya!

Mnafiki hana haya, njaa inavyomsumbua,
Hata chini atakaa, msala mchafu ukiwa,
Apate kunyenyekea, ili kuja kutumbua,
Mnafiki hana haya, huvaa yanayompwaya!

Ila wanaomtambua. pembeni humwangalia,
Jicho kumkodela, na tabia kushangaa,
Kwake huwa yasokuwa, na yalokuwa kupwaya,
Mnafiki hana haya, huvaa yanayompwaya!

Mshairi nang'amua, kwa watu kuangalia,
Imejijenga tabia, ya unafiki na riha,
Watu wafanza nazaa, na mengi yasiyofaa,
Mnafiki hana haya, huvaa yanayompwaya!

Na wengine hudhania, siku yao waijua,
Ya wengine kulilia, ambayo hawatapewa,
Na wakija kugundua, njaa imewahadaa,
Mnafiki hana haya, huvaa yanayompwaya!

Mtu wa kuhurumiwa, mnafiki alokuwa,
Heshima itampoteya, na gamba akavuliwa,
Kama kuku naye pia, haachi kunyonyolewa,
Mnafiki hana haya, huvaa yanayompwaya!

Naogopa domokaya, wao mtu humdhania,
Kisha wakamuambia, ukweli yasiyokuwa.
Na mjinga akijua, mwerevu anafulia,
Mnafiki hana haya, huvaa yanayompwaya!


Februari 8. 2012,
Dar es Salaam.

No comments: