Wewe sio sungusungu, toa machoni ukungu,
Halijawa lako fungu, asilolipanga Mungu,
Ukisikia uchungu, si kuzaa wanguwangu,
Washindwa taa za Mungu, utaweza ya Mzungu?
Jua laangaza mbingu, mchana ni lake fungu,
Na mwezi kwenye mawingu, usipofanyiwa mzungu,
Alijua hata bungu, kwalo amshukuru Mungu,
Washindwa taa za Mungu, utaweza ya Mzungu?
Mhindi kampe dengu, dona ndio langu fungu,
Chako sikifanyi changu, kwa utamu na utungu,
Sihofu kizunguzungu, yakidorora mawingu,
Washindwa taa za Mungu, utaweza ya Mzungu?
Figo halijawa wengu, sio wasiwasi wangu,
Mbona mwapika majungu, kwa lisilo lenu fungu,
Yenu, yenu, yangu, yangu, wanilia nini kungu?
Washindwa taa za Mungu, utaweza ya Mzungu?
Huzai una uchungu, au wafanza mizungu ?
Yaliyo kwenye uvungu, kayaweke kwenye chungu,
Na unapomla ningu, miba itoe kwa fungu,
Washindwa taa za Mungu, utaweza ya Mzungu?
Usijejifunga pingu, kifungo kina utungu,
Omba ukwepe marungu, ya watakao uungu,
Chini litaraji fungu, kibua haitwi changu,
Washindwa taa za Mungu, utaweza ya Mzungu?
Siku zako sio zangu, kuwa kadiri mwanangu,
Wanhyonge uwape fungu, katika yako mafungu,
Wala usiwe mchungu, hiyo siyo radhi yangu,
Washindwa taa za Mungu, utaweza ya Mzungu?
Firdausi kuwa fungu, nakushauri mwanangu,
Usijitie ya Wazungu, yakakupata machungu,
Pepo kuanzia kwangu, juu namwachia Mungu,
Washindwa taa zJua Mungu, utaweza ya Mzungu?
Februari 8. 2012,
Dar es Salaam.
Monday, February 6, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment