SAFARI hufiki mbali, ukongozwa na njaa,
Ukaikosa akili, na wazungu kukuhadaa,
Wakakufanza anzali, akili hukuchezea,
Ukiongozwa na njaa, safari hufiki mbali?
Matajiri huwavaa, wengi wakawanunua,
Mfukoni kuwatia, kulhali kuwatumia,
Wasiweze jizuia, tamaa ikiingia,
Ukiongozwa na njaa, safari hufiki mbali?
Humanya dh'ofu kulhali, wakaganga yako njaa,
Utapewa penseli, wakachukukua risasi,
Hukugawia bakuli, uranium wakatwaa,
Ukiongozwa na njaa, safari hufiki mbali?
Dhahabu huzozwa ghali, wageni wakaikuchukua,
Wakawapa mabangili, nanyi mkayaringia,
Kwa kuikosa akili, nchi haitoendelea,
Ukiongozwa na njaa, safari hufiki mbali?
Njaa yazidi ukali, na chama kinafulia,
Subira sio kauli, kwao hawataridhia,
Watafanza bilkuli, haramu kuichukua,
Ukiongozwa na njaa, safari hufiki mbali?
Pipi huiona ghali, zuzu ikawavutia,
Haluwa ikawa mali, wasisite kuchukua,
Wakaingia udhalili, viumbe wasiojaliwa,
Ukiongozwa na njaa, safari hufiki mbali?
Watatoa vya halali, mara elfu vilokuwa,
Nao kuonja asali, mara moja kuachiwa,
Daawa ya baradhuli, si watu wa kuhurumia,
Ukiongozwa na njaa, safari hufiki mbali?
Hutoshwa na maankuli, arshi wakaiachia,
Hujifanza mabahili, kwa wazawa wakijua,
Ila wakifika nduli, bei rahisi huachia,
Ukiongozwa na njaa, safari hufiki mbali?
Mshairi sina hali, nchi yangu nalilia,
Naona kama kandili, utambi unaofifia,
Dhila na idhilali, nyingi ninatarajia,
Ukiongozwa na njaa, safari hufiki mbali?
Sasa kunazo dalili, ndiyo hapa twafikia,
Hii ni kubwa ajali, lazima kujiokoa,
La sivyo ardhilhali, maovu yategemewa,
Ukiongozwa na njaa, safari hufiki mbali?
Hawaipati jamali, mamluki wenye njaa,
Maovu kuyakabili, hatamu kwao hujakuwa,
Wasipende vya halali, vya dhalimu kupakua,
Ukiongozwa na njaa, safari hufiki mbali?
Hawanayo maadili, ni matumbo huamua,
Ni watu kiwiliwili, kiakili ni kinyaa,
Utu wao si kamili, shetani kauchukua,
Ukiongozwa na njaa, safari hufiki mbali?
Tumuombeni Jalali, hata kutuondolea,
Tukabki na asili, na utu waliokuwa,
Nchi ipate amali, na Mola kuiangalia,
Ukiongozwa na njaa, safari hufiki mbali?
Kwa mchana na laili, watu kutokupota,
Njia ya kweli kukabili, hadi mwisho kufanikiwa,
UKawa mustakabli, ni mwema uliokuwa,
Ukiongozwa na njaa, safari hufiki mbali?
Si wa posho na nauli, njaa wanaokataa,
Hufanya yenye adili, hata wakajitolea,
Maisha kwao si ghali, na dunia huhofia,
Ukiongozwa na njaa, safari hufiki mbali?
Nadra kustahimili, wakionewa raia,
Huziba zao akili, wakashindwa kuelewa,
Na hutanuka musuli, kutaka kusaidia,
Ukiongozwa na njaa, safari hufiki mbali?
Hawa ni watu wa kweli, si watu wa kujitia,
Huithamini kauli, na ukweli kuulea,
Huitumia akili, si umbeya na kuzomea,
Ukiongozwa na njaa, safari hufiki mbali?
No comments:
Post a Comment