Friday, February 17, 2012

Mnafiki hubomoa

Mnafiki hutumiwa, na wa ndani na nje pia,
Ya kwao yakachanua, kwa malengo kuwafaa,
Na yeye ni kitambaa, makamasi huachiwa,
Mnafiki hubomoa, sikuzote si mjenzi,
Na hasa anapokuwa, ni wa watu kiongozi,
Ni kiraka cha mikogo,
Hutumiwa na vigogo,
Ni karatasi ya choo,
Hutumiwa na vizito!

Udogoni huanzia, sio tu anapokuwa,
Utashi humuishia, wengine kuwangojea,
Hutumwa akakimbia, hata asikokujua,
Mnafiki hubomoa, sikuzote si mjenzi,
Na hasa anapokuwa, ni wa watu kiongozi,
Ni kiraka cha mikogo,
Hutumiwa na vigogo,
Ni karatasi ya choo,
Hutumiwa na vizito!

Uzuzi kwake huvia, hana analochambua,
Sembuse kuja ng'amua, au baya kuligundua,
Huishi kwa majaliwa, kaburini kumtia,
Mnafiki hubomoa, sikuzote si mjenzi,
Na hasa anapokuwa, ni wa watu kiongozi,
Ni kiraka cha mikogo,
Hutumiwa na vigogo,
Ni karatasi ya choo,
Hutumiwa na vizito!

Sio wa kutegmewa, sembuse kujaaminiwa,
Yake ukimsikia, jua wenda kupotea,
Analolifikiria, ni wewe kununuliwa,
Mnafiki hubomoa, sikuzote si mjenzi,
Na hasa anapokuwa, ni wa watu kiongozi,
Ni kiraka cha mikogo,
Hutumiwa na vigogo,
Ni karatasi ya choo,
Hutumiwa na vizito!

Utumwani atawatia, hata macho walokua,
Wakijakushtukia, minyororo wamevaa,
Wakawa waning'inia, wasijue pakwachia,
Mnafiki hubomoa, sikuzote si mjenzi,
Na hasa anapokuwa, ni wa watu kiongozi,
Ni kiraka cha mikogo,
Hutumiwa na vigogo,
Ni karatasi ya choo,
Hutumiwa na vizito!

Hata wakubwa wakiwa, ni watu wa kutumiwa,
Ninawasikitikia, watu wasiojitambua,
Na kizazi kilokuwa, huruma kuwaonea,
Mnafiki hubomoa, sikuzote si mjenzi,
Na hasa anapokuwa, ni wa watu kiongozi,
Ni kiraka cha mikogo,
Hutumiwa na vigogo,
Ni karatasi ya choo,
Hutumiwa na vizito!

Yarabi nakulilia, utumwa kutonitia,
Kwa juu waliokuwa, hali ninajitambua,
Ni heri kunichukua, kuliko hivyo ikawa,
Mnafiki hubomoa, sikuzote si mjenzi,
Na hasa anapokuwa, ni wa watu kiongozi,
Ni kiraka cha mikogo,
Hutumiwa na vigogo,
Ni karatasi ya choo,
Hutumiwa na vizito!

No comments: