HAUBAKIZI ukoko, upako ukipakua,
Nusura si miondoko, na kunena majaliwa,
Kiumbe ana vituko, hasa anapojaliwa,
Upako ukipakua, haubakizi ukoko!
Wenza huona ukoko, kila anapopakua,
Hupakua bila mwiko, mwenyewe akajijazia,
Akadhihaki mauko, na siku ya kuugua,
Upako ukipakua, haubakizi ukoko!
Kwangu hubaki kicheko, mnya kisa anayakua,
Buza hata nako Boko, wote wameshamjua,
Sanaa yake mikoko, isiyoalika maua,
Upako ukipakua, haubakizi ukoko!
Maombi kwangu zindiko, ila mmoja yakiwa,
Hapa huwa mshtuko, akili zikatulia,
Wengine ni mafuriko, wenda mbali kuwazoa,
Upako ukipakua, haubakizi ukoko!
Haya ghali maandiko, hujuu ukiridhiwa,
Huwa pema waitwako, wanaoiona njia,
Wengine wote ni mwiko, milele hawataijua,
Upako ukipakua, haubakizi ukoko!
Hupwaya misukosuko, na nanga kushikilia,
Wote wenye hangaiko, bandarini hupwelea,
Wakapata angaziko, ukweli wakishajua,
Upako ukipakua, haubakizi ukoko!
Madaktari mliko, dua ninawaombea,
Mola kati yenu yuko, kwa uongo kusingiziwa,
Tunavijua vituko, vya walionunuliwa,
Upako ukipakua, haubakizi ukoko!
Utakuja mshtuko, mikononi kutulia,
Kwenye huo mpasuko, wenyewe mtayaamua,
Lisiwe ni fadhaiko, ahadi itatimia,
Upako ukipakua, haubakizi ukoko!
Namshukuru aliko, dhaifu namlilia,
Ukweli kwangu tambiko, na haki naihofia,
Kauli nyingine bako, wabwabwajao huvia,
Upako ukipakua, haubakizi ukoko!
No comments:
Post a Comment