Monday, February 13, 2012

Matajiri kutulea?

Matajiri mwawaachia,
Masikini kutulea,
Ninabki nashangaa,
Jinsi itakavyokuwa,
Kujakuwa lisilokuwa,
Fukara kufarijiwa:
Wema mliojaliwa, waovu mwawaachia,
Kwa kuwa mwanunuliwa, vijisenti mkapewa,
Nchi mkaiachia, mbwamwitu kuchukua,
Vizazi vitawahukumu, peponi kutoingia!

Vyama vyetu vyapotea,
Matajiri kuridhia,
Mikopo kuichukua,
Na hisani kuwania,
Kisha deni kugeuziwa,
Hadi mwisho wa dunia:
Wema mliojaliwa, waovu mwawaachia,
Kwa kuwa mwanunuliwa, vijisenti mkapewa,
Nchi mkaiachia, mbwamwitu kuchukua,
Vizazi vitawahukumu, peponi kutoingia!

Uongozi ni sanaa,
Na sayansi kutumia,
Mkuu ukitumiwa,
Nchi huja nunuliwa,
Ikauzwa waangalia,
Na kauli kutotoa:
Wema mliojaliwa, waovu mwawaachia,
Kwa kuwa mwanunuliwa, vijisenti mkapewa,
Nchi mkaiachia, mbwamwitu kuchukua,
Vizazi vitawahukumu, peponi kutoingia!

Haya yameanza mwaa,
Mwisho mwii yatakuwa,
Wakubwa wasipojijua,
Kaburi hujichimbia,
Na ndiyo yanayokuwa,
Wala hatujajitambua:
Wema mliojaliwa, waovu mwawaachia,
Kwa kuwa mwanunuliwa, vijisenti mkapewa,
Nchi mkaiachia, mbwamwitu kuchukua,
Vizazi vitawahukumu, peponi kutoingia!

Nabii wanaojizaa,
Hawawezi saidia,
Njaa inawasumbua,
Na moto kufakamia,
Mola wanamtania,
Na wengine kuhukumu:
Wema mliojaliwa, waovu mwawaachia,
Kwa kuwa mwanunuliwa, vijisenti mkapewa,
Nchi mkaiachia, mbwamwitu kuchukua,
Vizazi vitawahukumu, peponi kutoingia!

Mbali hawatafikia,
Katikati huishia,
Ikashuka yakufaa
Kusahau kutokuwa,
Na siku ikiwadia,
Wala hawataijua:
Wema mliojaliwa, waovu mwawaachia,
Kwa kuwa mwanunuliwa, vijisenti mkapewa,
Nchi mkaiachia, mbwamwitu kuchukua,
Vizazi vitawahukumu, peponi kutoingia!

Wengine kweli vichaa,
Mbwa keshajing'atia,
Husema wasiyojua,
Na hujua wasojua,
Vifua wakaifua,
Kumbe wanajifulia:
Wema mliojaliwa, waovu mwawaachia,
Kwa kuwa mwanunuliwa, vijisenti mkapewa,
Nchi mkaiachia, mbwamwitu kuchukua,
Vizazi vitawahukumu, peponi kutoingia!

Watu wakusikitia,
Utume wanaoutwaa,
Na watukufu wakawa,
Kumbe uchafu wajaa,
Na Mola anayajua,
Na yeye awangojea:
Wema mliojaliwa, waovu mwawaachia,
Kwa kuwa mwanunuliwa, vijisenti mkapewa,
Nchi mkaiachia, mbwamwitu kuchukua,
Vizazi vitawahukumu, peponi kutoingia!

Nitunze moyo radhia,
Hofu uliotangulia,
Na chini unaokaa,
Na mbele kutosogea,
Udhalili nalilia,
Kesho kuja ninyanyua:
Wema mliojaliwa, waovu mwawaachia,
Kwa kuwa mwanunuliwa, vijisenti mkapewa,
Nchi mkaiachia, mbwamwitu kuchukua,
Vizazi vitawahukumu, peponi kutoingia!

Mengine sintoridhia,
Miye naweza kimbia,
Nautamani ukiwa,
Peke yangu nikakaa,
Iwe nakuangukia,
Toba kunikubalia:
Wema mliojaliwa, waovu mwawaachia,
Kwa kuwa mwanunuliwa, vijisenti mkapewa,
Nchi mkaiachia, mbwamwitu kuchukua,
Vizazi vitawahukumu, peponi kutoingia!

Ni dhaifu nimekuwa,
Baada ya kukujua,
Mmoja uliyekuwa,
Na wengine ni bandia,
Inshallah ninaitoa,
Yangu kuyafikiria:
Wema mliojaliwa, waovu mwawaachia,
Kwa kuwa mwanunuliwa, vijisenti mkapewa,
Nchi mkaiachia, mbwamwitu kuchukua,
Vizazi vitawahukumu, peponi kutoingia!

Mwisho mwema kuujua,
Na shahada kuitoa,
Na ulimi kutambua,
Ni mmoja uliyekuwa,
NIsishindwe na hadaa,
Mengine kukuzulia:
Wema mliojaliwa, waovu mwawaachia,
Kwa kuwa mwanunuliwa, vijisenti mkapewa,
Nchi mkaiachia, mbwamwitu kuchukua,
Vizazi vitawahukumu, peponi kutoingia!

No comments: