Monday, February 6, 2012

Ngoma iko kileleni

Ngoma iko kileleni, na kelele zimewini,
Watu hawasikizani, utamu wa nje na ndani,
Pepo wako mitaani, watoka usingizini,
Mwapayuka kitu gani,
Kwenye kelele ngomani,
Mbona hatuelewani,
Mnataka kitu gani,
Au tuko hatarini,
Na siyo tunaojua?

Waume wako ngomani, na mikono viunoni i,
Wanawake si gauni, ni sketi za majani,
Vya nje tunathamini, na siyo zetu imani,
Mwapayuka kitu gani,
Kwenye kelele ngomani,
Mbona hatuelewani,
Mnataka kitu gani,
Au tuko hatarini,
Na siyo tunaojua?


Na walio madarakani, wajinga wamebaini,
Mtu kugeuzwa nyani, huu mbaya utani,
Unadumu uzaini, watu wangali gizani,
Mwapayuka kitu gani,
Kwenye kelele ngomani,
Mbona hatuelewani,
Mnataka kitu gani,
Au tuko hatarini,
Na siyo tunaojua?

Ngoma iko kileleni, mnasema kitu gani,
Sasa shingo viunoni, sasa zaanguka chini,
Zasagika mchangani, rangi za pinde kuwini,
Mwapayuka kitu gani,
Kwenye kelele ngomani,
Mbona hatuelewani,
Mnataka kitu gani,
Au tuko hatarini,
Na siyo tunaojua?

Lazidi jasho mwilini, michirizi waniwani,
Utadhani maji mtoni, au mferejini,
Watu tena hawaoni, jasho lazidi machoni,
Mwapayuka kitu gani,
Kwenye kelele ngomani,
Mbona hatuelewani,
Mnataka kitu gani,
Au tuko hatarini,
Na siyo tunaojua?

Vigelegele ngomani, vyasikika ugenini,
Na mingurumo yaghani, tetemeko chinichini,
Msukosuko moyoni, kila mtu yu peponi,
Mwapayuka kitu gani,
Kwenye kelele ngomani,
Mbona hatuelewani,
Mnataka kitu gani,
Au tuko hatarini,
Na siyo tunaojua?

Wenyewe hawaonani, macho yatazama ndani,
Yazizima afueni, kwa damu masikioni,
Milizamu ikibuni, njia mpya usoni,
Mwapayuka kitu gani,
Kwenye kelele ngomani,
Mbona hatuelewani,
Mnataka kitu gani,
Au tuko hatarini,
Na siyo tunaojua?

Nywele kote vifuatni, zaloa sio utani,
Jasho linashuka chini, bila kikwazo mwilini,
Laabiri miguuni, na kwingia vidoleni,
Mwapayuka kitu gani,
Kwenye kelele ngomani,
Mbona hatuelewani,
Mnataka kitu gani,
Au tuko hatarini,
Na siyo tunaojua?

Watu wako furahani, na hapa si msibani,
Nyie mwateta ya nini, tena hapa kilingeni,
Hamchezi mwafanyani, mwataka twambia nini,
Mwapayuka kitu gani,
Kwenye kelele ngomani,
Mbona hatuelewani,
Mnataka kitu gani,
Au tuko hatarini,
Na siyo tunaojua?

Nzi kufa kidondani, ladumu toka zamani,
Mwafrika msanii, hili analithamini,
Mauti kuja ngomani,
mizimu huwa auni,
Mwapayuka kitu gani,
Kwenye kelele ngomani,
Mbona hatuelewani,
Mnataka kitu gani,
Au tuko hatarini,
Na siyo tunaojua?

Hamchezi nje nendeni, tuonane kesho jioni,
Kuna wakati kazini, na wakati wa rahani,
Kuchagua kitu gani, kama kesho huthamini?
Mwapayuka kitu gani,
Kwenye kelele ngomani,
Mbona hatuelewani,
Mnataka kitu gani,
Au tuko hatarini,
Na siyo tunaojua?

Walewa hadi kopeni, manju wachanganyikiwa,
Wasikie kitu gani, ila raha kutambaa,
Kwao kingine yumkini, kesho hawatakijua,
Mwapayuka kitu gani,
Kwenye kelele ngomani,
Mbona hatuelewani,
Mnataka kitu gani,
Au tuko hatarini,
Na siyo tunaojua?

Februari 8. 2012,
Dar es Salaam.

No comments: