Watu ovyo watetema, nyumbani kuna zahama,
Waliwa watu wazima, kama vile ni wanyama,
Nunda roho azigema, kama pombe ya mtama,
Nunda mla mbuzi kafa, kaja nunda mla watu!
Waogopa kina mama, kwenda kunako kisima,
Maji sasa tunakwama, mikojo tunaichuma,
Zinaondoka ghanima, na kutwambaa rehema,
Nunda mla mbuzi kafa, kaja nunda mla watu!
Nunda nuru huizima, hata mchana kuzima,
Kila anapochutama, akiruka ana ndama,
Ni ndama mtu mzima, si mwana ng'ombe nasema,
Nunda mla mbuzi kafa, kaja nunda mla watu!
Walia watu wazima, hata wana usalama,
Wanakiona kiyama, nje yao chasimama,
Waitafuta huruma, nunda hana la kusema,
Nunda mla mbuzi kafa, kaja nunda mla watu!
Si paka wa kuazima, au chui wa kutuma,
Huyu nunda twamsema, hivi sasa kumbe chama,
Kumbe yote hii nakama, chanzo yeye yanavuma,
Nunda mla mbuzi kafa, kaja nunda mla watu!
Nchi washindwa tazama, ukubwa wanausoma,
Na mbumbumbu kuwatuma, yasiyosemwa kusema,
Hasira zinanguruma, mioyo imepindama,
Nunda mla mbuzi kafa, kaja nunda mla watu!
Nakama iwe nakama, watu waanza kusema,
Kugeuzwa maamuma, na dini wasiosoma,
Haya yataka utumwa, hadimu nao wagoma,
Nunda mla mbuzi kafa, kaja nunda mla watu!
Kibaya sasa ni chema, na wao kujitazama,
Vioo vimeparama, wazuri wanajinoma,
Nchi yazidi kuzama, hakuna wa kusukuma,
Nunda mla mbuzi kafa, kaja nunda mla watu!
Na mtumwa keshazama, kwenye mfuko kuchuma,
Mtumaji alalama, uwapi mlishonyuma ?
Hakika ya kuazima, nguo haiwi neema,
Nunda mla mbuzi kafa, kaja nunda mla watu!
Februari 6, 2012,
Dar es salaam.
Monday, February 6, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment