Monday, February 6, 2012

Kutaka kitu kingine

Unalopanga huvia, yakaja usiyojua,
We panga na kupangua, hujui lijalo kuwa,
Kesho wanayonuia, yaweza kuwakataa,
Kutaka kitu kingine, kufanikisha kingine!

Imani waliopwaya, wajanja wa kutazamia,
Kwa waganga waambiwa, ni wakati wa kugombea,
Mkenge wanaingia, wengi wasiojijua,
Kutaka kitu kingine, kufanikisha kingine!

Mola akijapangua, na mganga kumwondoa,
Nini litalobakia, kwa nguzo kuondolewa,
Wajinga nawashangaa, watu wanavyozainiwa,
Kutaka kitu kingine, kufanikisha kingine!

Kutaka ukiamua, waweza kujitakia,
Ila kuja fanikiwa, si lazima kuja kuwa,
Alaa ukishamjua, huweka nyengine gia,
Kutaka kitu kingine, kufanikisha kingine!

Inshallah hutangulia, akaanza kuitoa,
Njia akachaguliwa, iwezayo kumfaa,
Akawa kafanikiwa, ya peponi na dunia,
Kutaka kitu kingine, kufanikisha kingine!

Jibari hujinyanyua, amri wakaitoa,
Firauni twamjua, na aliyoazimia,
Yake kamwe hayakuwa, Qadiri akamtwaa,
Kutaka kitu kingine, kufanikisha kingine!

Naomba kuahidiwa, kutaka kutokujaliwa,
Najua wake udhia, nilivyouvumilia,
Yatosha yaliyo dia, hadi nitaporejea,
Kutaka kitu kingine, kufanikisha kingine!

Nipe kinachonifaa, halali nikachukua,
Niepushe na balaa, cha haramu kuchukua,
Nikeshe kuhimidia, na sifa kukumwaiya,
Kutaka kitu kingine, kufanikisha kingine!

Februari 8, 2012,
Dar es Salaam.

No comments: