Na nilikuangalia, na kutaka kukulea,
Mjinga kwako nikawa, na kubasi la kuvua,
Yangu uliyakataa, ya ngoroko kuchukua,
Jeuri imekuponza, mwenyewe wajiumiza!
Jeui ukajitia, na matusi kukujaa,
Dharau ukaivaa, na shanga kuivalia,
Nami kimya nikakaa, siku nikiingojea,
Jeuri imekuponza, mwenyewe wajiumiza!
Muda haukuchelewa, miaka ikafikia,
Uhuru ulipokuwa, na waoto wamekua,
Hukujua nangojea, ulidhani natania,
Jeuri imekuponza, mwenyewe wajiumiza!
Ulikuwa ni kichaa, mtu usiyesikia,
Yako kujifanyia, yasiyowapendezea,
Na laana kufukua, na wana kuwatupia,
Jeuri imekuponza, mwenyewe wajiumiza!
Mapenzi hukujaliwa, ila wabeba sanaa,
Kila kitu kujitia, wajua usiyejua,
Wengi wakakushangaa, ujinga uliovaa,
Jeuri imekuponza, mwenyewe wajiumiza!
Juzuu kukazania, sasa unattakiwa,
Sura Na'ba kuijua, dua ukaiombea,
Maradhi kukupungua, kichwani yalokujaa,
Jeuri imekuponza, mwenyewe wajiumiza!
Na jeneza kuzuia, wana lisije chukua,
Wazee wako yafaa, kinga kuwaulizia,
Upuuzi uliotoa, madhara kutotokea,
Jeuri imekuponza, mwenyewe wajiumiza!
Ni mpweke nitakuwa, ila kensa naitoa,
Pengine nitafikiria, madeni ukilipiwa,
Nyumbani ukarejea, mama wa nyumbani kuwa,
Jeuri imekuponza, mwenyewe wajiumiza!
Biashara nakataa, marufuku kuijua,
Ila vitu kuandaa, nyumbani unapokuwa,
Na mikopo kuchukua, si ruhusa nakwambia,
Jeuri imekuponza, mwenyewe wajiumiza!
Wataka waharibia, wana wangali wakua,
Msingi kumalizia, chini wote kuishia,
Hakika wakosa haya, kisirani umekuwa,
Jeuri imekuponza, mwenyewe wajiumiza!
Na jeuri wajitia, kujifanya waonewa,
Mwisho umeshafikia, ukweli tunaujua,
Wengi umewaibia, siku zote wanalia,
Jeuri imekuponza, mwenyewe wajiumiza!
Nakuomba angukia, ndugu kukusaidia,
Mikopo uliyochukua, na wizi ulokuwa,
Madeni kukulipia, salama upate kuwa,
Jeuri imekuponza, mwenyewe wajiumiza!
No comments:
Post a Comment