Monday, February 6, 2012

Ni msimamo wa chama

Katiba kupinduliwa, ni msimamo wa chama,
Ya Mussa ukishangaa, ya Farao hujasoma,
Ukuu waliopewa, sasa wako juu ya umma,
Mambo yakienda kombo, ni msimamo wa chama!

Wananchi kuwahadaa, na kauli kuwazima,
Haya yameshatokea, na sasa mwaka mzima,
Wamelala walokua, kwenye kitanda cha chama,
Mambo yakienda kombo, ni msimamo wa chama!

Uchama kitu adawa, hupasuka nchi nzima,
Ubaguzi ukazua, wa chama na waso chama,
Wao wakajipendelea, na kuzifanya dhuluma,
Mambo yakienda kombo, ni msimamo wa chama!

Ubinafsi hukua, ndani na nje ya chama,
Watu kujichukulia, hata mali yake umma,
Pasiwe cha kubakia, ila kujaza tuhuma,
Mambo yakienda kombo, ni msimamo wa chama!

Kazibure watapewa, mengi yenye uadhama,
Kimya wakapokea, hiyo yao takrima,
Neema kwao ikawa, wakazama maamuma,
Mambo yakienda kombo, ni msimamo wa chama!

Uchama una hatia, tena na kubwa gharama,
Itazikwa Tanzania, kwa kutetea ya chama,
Nchi wakaiachia, mamboye yende mrama,
Mambo yakienda kombo, ni msimamo wa chama!

Kwingneko angalia, Misri nako tazama,
Chama kilivyowaparua, na uhai kuuzima,
Hatihati imekuwa, hadi leo haijakoma,
Mambo yakienda kombo, ni msimamo wa chama!

Uchama ukiamua, hulinda wenye tuhuma,
Wezi ikawatetea, na kuachia dhuluma,
Na dhambi zikaenea, mikoa na nchi nzima,
Mambo yakienda kombo, ni msimamo wa chama!

Waovu wataachiwa, uongozi kuufuma,
Wengi wakanunuliwa, uhadimu kujitoma,
Nchi ikalaaniwa, na mambo yake kukwama,
Mambo yakienda kombo, ni msimamo wa chama!

Februari 7, 2012
Dar es Salaam.

No comments: