Vyama vingi vinakua, na mapishi yanukia,
Mseto unatakiwa, mapochopocho kutua,
Wa zamani waishiwa, kwa hoja kuwapotea,
Mseto wa Tanganyika, nauliza uko wapi?
Sasa wanashikila, uhai milele kuwa,
Yamewaparaganyikia, sasa wachanganyikiwa,
Hakuna nyengine dawa, ni mseto kutumia,
Mseto wa Tanganyika, nauliza uko wapi?
Itaondoa malaria, kwa wale wanaosinzia,
Vilimilimi kumea, kukaisha kuzomea,
Vigelegele kuvia, wajinga tukawajua,
Mseto wa Tanganyika, nauliza uko wapi?
Mkoko waitikia, umealika maua,
Vyama vyainukia, watoto waliokuwa,
Sasa wakubwa wapwaya, hoja zimewapotea,
Mseto wa Tanganyika, nauliza uko wapi?
Ghasia tunajazia, watu zisizowafaa,
Ni wale wanaozubaa, na ukubwa kujitia,
Wakaishia kuachiwa, ghorofa kushikilia,
Mseto wa Tanganyika, nauliza uko wapi?
Kuna wasoma sheria, vifungu wanapangua,
Ni mengi wanayojua, waishiwa kuzomewa,
Afkani wadhania, watu wazima wapea,
Mseto wa Tanganyika, nauliza uko wapi?
Majina ningewatajia, naogopa kukamiwa,
Wenyewe mtachagua, kusuka au kunyoa,
Ila wakati najua, hakika umewadia,
Mseto wa Tanganyika, nauliza uko wapi?
Maharage kuchagua, au kunde zinafaa,
Na mchele kuchukua, uchafu ukaondoa,
Kisha kuchanganyia, mseto safi ukawa,
Mseto wa Tanganyika, nauliza uko wapi?
Wali tunaopikiwa, mawe ndani umejaa,
Hawana la kuchagua, kila kitu waridhia,
Yanahofia balaa, meno yachanganyikiwa,
Mseto wa Tanganyika, nauliza uko wapi?
Wali umeshafubaa, nazi wala haukutiwa,
Mkaa waliotumia, hakika ulipungua,
Ni mbichi uliokuwa, tunashindwa kujilia,
Mseto wa Tanganyika, nauliza uko wapi?
Mseto kujipikia, nafaka tutachagua,
Taka zote kuondoa, salama seto likawa,
Wata kwa zao raha, chakula wakakivaa,
Mseto wa Tanganyika, nauliza uko wapi?
Februari 8, 2012,
Dar es Salaam.
Monday, February 6, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment