Friday, February 17, 2012

Mwapiga ngoma ya kifo

Uroho utatuumbua, na tamaa kutuua,
Wamiliki watakiwa, kujenga kisha kukaa,
Madini wanakochimbua, wao na zao jamaa,
Mwapiga ngoma ya kifo, kucheza acheze nani?
Walemavu tukizaa,
Na kojale umauti?
Haiwezi kuwa hoja

Viongozi nao pia, haya wanaoridhia,
Si wajinga kuwavaa, na kisha mkawahadaa,
Njaa inayowasumbua, kitu wasiokijua,
Mwapiga ngoma ya kifo, kucheza acheze nani?
Walemavu tukizaa,
Na kojale umauti?
Haiwezi kuwa hoja

Nchi haijajiandaa, maafa mwatuletea,
Ya kawaida mwazubaa, makubwa yasiwe baa,
Mbona twawaajabia, ovyo kukeungikiwa,
Mwapiga ngoma ya kifo, kucheza acheze nani?
Walemavu tukizaa,
Na kojale umauti?
Haiwezi kuwa hoja

Njaa mnailea, utajiri mwawania?
Umauti mkitia, wenzetu Watanzania,
Haya mtafurahia, mkala na kutanua?
Mwapiga ngoma ya kifo, kucheza acheze nani?
Walemavu tukizaa,
Na kojale umauti?
Haiwezi kuwa hoja

Macho mnayazuia, ukweli kuangalia,
Nyani mnamuua, kwa kinyume kumjia?
Laana mnaifungua, na kwenu haitaishia,
Mwapiga ngoma ya kifo, kucheza acheze nani?
Walemavu tukizaa,
Na kojale umauti?
Haiwezi kuwa hoja

Subira inatakiwa,siotunavyoingia,
Hujayakatupalia,puazijekuumia,
Pasiwewa kumlilia, nuksi tukizizaa,
Mwapiga ngoma ya kifo, kucheza acheze nani?
Walemavu tukizaa,
Na kojale umauti?
Haiwezi kuwa hoja

Pwani wanaotamia, nakovisiwani pia,
Hawawezi kuumia, haya watayasikia,
Bara waliochimbiwa, mizizi ikafukuliwa,
Mwapiga ngoma ya kifo, kucheza acheze nani?
Walemavu tukizaa,
Na kojale umauti?
Haiwezi kuwa hoja

Ngoma hii kuiondoa, tunaiomba dunia,
Waweze kusaidia, vingine kuganga njaa,
Wakati haujawadia, mabomu kuyachezea,
Mwapiga ngoma ya kifo, kucheza acheze nani?
Walemavu tukizaa,
Na kojale umauti?
Haiwezi kuwa hoja

Sumu haina radhia, wala wa kumuachia,
Pale inapoingia, damu zote zitalia,
Na vizazi kufatia, kama ilivyo India,
Mwapiga ngoma ya kifo, kucheza acheze nani?
Walemavu tukizaa,
Na kojale umauti?
Haiwezi kuwa hoja

Mshairi naachia, wengine kuendelea,
Sio vita ya mmoya, wanaharakati wajua,
Na wajinga wasojua, budi ukweli kujua,
Mwapiga ngoma ya kifo, kucheza acheze nani?
Walemavu tukizaa,
Na kojale umauti?
Haiwezi kuwa hoja

No comments: