Monday, February 6, 2012

Kiongozi na masikini

Kiongozi Mwafrika, ufukara autaka,
Kwake silaha hakika, kuyashika madaraka,
Nyie mwafanya dhihaka, ufukara kufutika?
Kiongozi na fukrara, uzee na mkongojo,
Bilavyo utang'olewa!

Mtunzi siachi cheka, kiongozi kumtaka,
Umaskini kuzika, ukawa nayo hakika,
Hili kuja kufanyika, na kweli ukatoweka,
Kiongozi na fukrara, uzee na mkongojo,
Bilavyo utang'olewa!

Nakataa nii dhihaka, Wazungu mnayotaka,
Ukimpa Mwafrika, kazi asiyoitaka,
Fedha akishazishika, vibarakala huweka,
Kiongozi na fukrara, uzee na mkongojo,
Bilavyo utang'olewa!

Na nyengine hutoweka, kama moshi zikafoka,
Mkewe akajitwika, na wanawe kuzipoka,
Makuwadi wakifika, mashimo huongezeka,
Kiongozi na fukrara, uzee na mkongojo,
Bilavyo utang'olewa!

Uongozi kuushika, njaa inahitajika,
Watu kuja kuhongeka, kidogo wakazuzuka,
Senti wakishazishika, kura yako ni hakika,
Kiongozi na fukrara, uzee na mkongojo,
Bilavyo utang'olewa!

Uungu wanautaka, kila linalofanyika,
Wajinga kutoshtuka, ni wao waliowaweka,
Na kila likijengeka, wapate wao sifika,
Kiongozi na fukrara, uzee na mkongojo,
Bilavyo utang'olewa!

Hata leo wanazuka, wenye akili mzuka,
Ukale umeibuka, yalyale wanashika,
Hili siachi shtuka, mambo yanavyoharibika,
Kiongozi na fukrara, uzee na mkongojo,
Bilavyo utang'olewa!

Mkongojo wautaka, viongozi Afrika,
Ufukara kuuweka, wayashike mamlaka,
Maana wakinyanyuka, wananchi watastuka,
Kiongozi na fukrara, uzee na mkongojo,
Bilavyo utang'olewa!

Tungo kamai huzikwa, watu macho kufungika,
Njaa yao kuridhika, ndivyo Mungu anavyotaka,
Kumbe wanadanganyika, ukombozi wautaka,
Kiongozi na fukrara, uzee na mkongojo,
Bilavyo utang'olewa!

Waganga wanapunjika, na walimu kadhalika,
Kusudi kutawalika, na dhuluma kufanyika,
Kisha wakigawanyika, ni rahisi kutumika,
Kiongozi na fukrara, uzee na mkongojo,
Bilavyo utang'olewa!

Nchi walioishika, na wabunge kadhalika,
Midomo inarefuka, na makucha kuongezeka,
Ili vizuri kubweka, kama kelbu wafugika,
Kiongozi na fukrara, uzee na mkongojo,
Bilavyo utang'olewa!

Dunia sasa hakika, vingine kuwajibika,
Misaada ikitoka, kwa wananchi kufika,
Nyumba zipate jengeka, ufukara kutoweka,
Kiongozi na fukrara, uzee na mkongojo,
Bilavyo utang'olewa!

Na kizazi kikizuka, siasa mpya kushika,
Nchi ipate jengeka, bila hila kuzishika,
Imani ikitoweka, wenyewe tutajizika,
Kiongozi na fukrara, uzee na mkongojo,
Bilavyo utang'olewa!

Februari 6, 2012
Dar es Salaam.

No comments: