Chama kushdrehekea, msibani kulokuwa,
Hujiuliza vichaa, au wameshalaniwa,
Kuahirisha yafaa, muhimu yasiyokuwa,
Mwiishiwa itikadi, huishi kwenye ya kale,
Kunukia ufisadi, ni marashi ya ndulele,
Historia ni kaidi, humtunuku mishale,
Afaidi ila idi,
Mwanakaya mkaidi!
Uhai kuutania, na maisha kuchezea,
Watu wachanganyikiwa, dhamana waliopewa,
Kupatiliza ikawa, daima ni yao dua,
Mwiishiwa itikadi, huishi kwenye ya kale,
Kunukia ufisadi, ni marashi ya ndulele,
Historia ni kaidi, humtunuku mishale,
Afaidi ila idi,
Mwanakaya mkaidi!
Mwiishiwa mheshimiwa, ukale hung'ang'ania,
Yake hayajatokea, kuganga ndwele ikawa,
Ovyo hujiropokea, asemayo kutojua,
Mwiishiwa itikadi, huishi kwenye ya kale,
Kunukia ufisadi, ni marashi ya ndulele,
Historia ni kaidi, humtunuku mishale,
Afaidi ila idi,
Mwanakaya mkaidi!
Juzi inshatangulia, ya kale yananukia?
Nyakati hujipindua, palepale wabakia,
Mawazo mgando baa, kwalo watu huangamia,
Mwiishiwa itikadi, huishi kwenye ya kale,
Kunukia ufisadi, ni marashi ya ndulele,
Historia ni kaidi, humtunuku mishale,
Afaidi ila idi,
Mwanakaya mkaidi!
Hali kuiangalia, busara kuitambua,
Kuna ya kuzungumzia, na yasiyozungumziwa,
Wakati kuuelewa, ni hekima kujaliwa,
Mwiishiwa itikadi, huishi kwenye ya kale,
Kunukia ufisadi, ni marashi ya ndulele,
Historia ni kaidi, humtunuku mishale,
Afaidi ila idi,
Mwanakaya mkaidi!
Wanaovimbisha vifua, msibani kulikofiwa,
Heshima imekimbia, na utu umepotea,
Si watu wanaojua, kwa wanayojifanyia,
Mwiishiwa itikadi, huishi kwenye ya kale,
Kunukia ufisadi, ni marashi ya ndulele,
Historia ni kaidi, humtunuku mishale,
Afaidi ila idi,
Mwanakaya mkaidi!
Vingine wamelaaniwa, huwezi kulizuia,
Siku inawangojea,nuchi njiani kukaa,
Wakwe kuwashangaa, waliovua kuvaa,
Mwiishiwa itikadi, huishi kwenye ya kale,
Kunukia ufisadi, ni marashi ya ndulele,
Historia ni kaidi, humtunuku mishale,
Afaidi ila idi,
Mwanakaya mkaidi!
Yapo ya kujiandaa, kwa jopo kulitumia,
Kauli kutoitoa, hadi lakusema wajua,
Mdomo ukiifungua,ni hakika walijua,
Mwiishiwa itikadi, huishi kwenye ya kale,
Kunukia ufisadi, ni marashi ya ndulele,
Historia ni kaidi, humtunuku mishale,
Afaidi ila idi,
Mwanakaya mkaidi!
Itikadi ukiishiwa, hufanya usiyojua,
'Kawa' kujiropokea, ikawa kama sheria,
Mtu ni kujitetea, ingawa keshapotea,
Mwiishiwa itikadi, huishi kwenye ya kale,
Kunukia ufisadi, ni marashi ya ndulele,
Historia ni kaidi, humtunuku mishale,
Afaidi ila idi,
Mwanakaya mkaidi!
Jalali mwonyesha njia, naomba kuniangalia,
Kila kipiga hatua, topeni kutoingia,
Na mawe kutojikwaa, salama nikarejea,
Mwiishiwa itikadi, huishi kwenye ya kale,
Kunukia ufisadi, ni marashi ya ndulele,
Historia ni kaidi, humtunuku mishale,
Afaidi ila idi,
Mwanakaya mkaidi!
Februari 6, 2012,
Dar es Salaam.
Monday, February 6, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment