Monday, February 20, 2012

Jeneza nalingojea

Mwenyewe nimesikia, kwangu hautorejea,
Na mtu sikuambiwa, maneno umeyatoa,
Na kiapo kuapia, hadi maiti ukiwa,
Jeneza nalingojea, ambalo wanitumia.

Maiti naikataa, haiwezi yangu kuwa,
Ila unayemfaa, sasa ulikotulia,
Yabadilika dunia, wakati umechelewa,
Jeneza nalingojea, ambalo wanitumia.

Hasira nazo ukiwa, waupata ukichaa,
Mwenzi nakusikitia, mumunye umeshakua,
Ukubwani yakupwaya, na kichekesho kwendakua,
Jeneza nalingojea, ambalo wanitumia.

Jeuri umezidia, na dharau kujitia,
Na hicho ulichokuwa, wengine wamejaliwa,
Tena wamezidishiwa, na kila mtu anajua,
Jeneza nalingojea, ambalo wanitumia.

Nani wa kukuhurumia, kiumbe usiyesikia,
Ubishi umekujaa, na vya watu kudokoa,
Urushi umeingia, na watu kusingizia,
Jeneza nalingojea, ambalo wanitumia.

Mikopo unachukua, biashara hujajua,
Hela zinakoendea, hakuna anayejua,
Mwanamke wapotea, au umeshachezewa,
Jeneza nalingojea, ambalo wanitumia.

Marafiki wachagua, mazuri wasokutakia,
Wajianya unajua, na sisi twakuachia,
Salama twajitakia, sio kuja kunadiwa,
Jeneza nalingojea, ambalo wanitumia.

Mwanamme kakuzuzua, hili hatujalijua,
Tabia twakushangaa, fedha zinavyopotea,
Mashimbo unatoboa, hata mitaji ikiwa,
Jeneza nalingojea, ambalo wanitumia.

Hakika weye balaa, sasa tumeshakujua,
Mbali na wewe kukaa, yabidi hivyo ikawa,
Vinginevyo kutulia, wazee wakikuombea,
Jeneza nalingojea, ambalo wanitumia.

Na laana kuitoa, uliyokwishajiwekea,
Jeneza kuaguliwa, mwingine kutochukua,
Ulimi hakika baa, waweza kuteketeya,
Jeneza nalingojea, ambalo wanitumia.

Waganga wakutambua, ATM umeshakua,
Wazidi kukufukua, tena na kukuchimbua,
Kiumbe unalaaniwa, kwa hayo unayozua,
Jeneza nalingojea, ambalo wanitumia.

Huruma nawaonea, wenye wake kama hawa,
Akili hukupasua, mengi ukamdhania,
Kumbe ameshalaniwa, huko anakotokea,
Jeneza nalingojea, ambalo wanitumia.

No comments: