Akili hukutumia, ingwa umejaliwa,
Bahati ukachezea, chooni ulipokuwa,
Shilingi kutumbukia, vyote vimeshapotea,
Kufata watu wa nje, wa ndani ukawabeza:
Nyongo yakutumbukia!
Ya mme hukusikia, kiburi ukajitia,
Na jeuri ukawa, kila alipokuongoa,
Heri ukaikataa, na shari kukurubia,
Kufata watu wa nje, wa ndani ukawabeza:
Nyongo yakutumbukia!
Wa nje kuwaendea, shirika kujifanyia,
Na waganga kuzoea, ushirikina kujaa,
Mkawa mwachanganyikiwa, mwazidi potea njia,
Kufata watu wa nje, wa ndani ukawabeza:
Nyongo yakutumbukia!
Wakowapi walokua, kila siku wasifia,
Kidume uliyekuwa, mume chini yako kawa,
Kumbe akuhesabia, siku yako kufikia,
Kufata watu wa nje, wa ndani ukawabeza:
Nyongo yakutumbukia!
Sura ulipuuzia, ila dini wajitia,
Kurani hukuijua, ubishi ulikujaa,
Na ulichoambulia, mwenyewe unakijua,
Kufata watu wa nje, wa ndani ukawabeza:
Nyongo yakutumbukia!
Un afiki kujitia, na uswalihina pia,
Kumbe nyoka ulikua, kichinichini wajia,
Kutuchoma kuamua, nyumbani tulokaa,
Kufata watu wa nje, wa ndani ukawabeza:
Nyongo yakutumbukia!
Dunia yakuumbua, mwanamke wa balaa,
Haya hukuitambua, nani kukuangalia,
Mola ukimrudia, pengine kukuafua,
Kufata watu wa nje, wa ndani ukawabeza:
Nyongo yakutumbukia!
Ushirikina kimbia, au unaangamia,
Na mume kumwangukia, ndiyo dawa itakuwa,
Vinginevyo twachomoa, akhera mbali pia kuwa,
Kufata watu wa nje, wa ndani ukawabeza:
Nyongo yakutumbukia!
Dhuluma kujifanyia, na urushi kuujua,
Sumu yake hukujua, wanao itawavaa,
Wajukuu nao pia, usipowarejeshea,
Kufata watu wa nje, wa ndani ukawabeza:
Nyongo yakutumbukia!
Rahma ungelikuwa, haya yasingetokea,
Ila kwa kukosa neema, ulizaliwa Rehema,
Tubu kisha ungamia,
Kufata watu wa nje, wa ndani ukawabeza:
Nyongo yakutumbukia!
No comments:
Post a Comment