Watu hawajawa mawe, nache na changu kibwebwe,
Mbwani wauliza weye, hujui yana wenyewe,
Ni vipanga nao mwewe, wengine kazi wanyowe,
Taifa kama kijiwe, viranja wanakijiwe!
Humeza ngozi na kowe, nani apige mayowe,
Kila mme na mkewe, na kila mke na mumewe,
Na mzazi na mwanawe, nchi ikawa isiwe,
Taifa kama kijiwe, viranja wanakijiwe!
Mbwani wapiga mayowe, wataka nini ujuwe,
Nchi inao wenyewe, na wala hujawa wewe,
Yafaa ukatibiwe, umeshikwa na kiwewe,
Taifa kama kijiwe, viranja wanakijiwe!
Hupewa wenye vijiwe, walokwishapanga mawe,
Robo tatu ya mwenyewe, robo wewe kachukue,
Kwa vipi upate wewe, ya nifae nikufae ?
Taifa kama kijiwe, viranja wanakijiwe!
Wanayajua Msewe, hadi wa kule Mbwewe,
Iwaje izaya weye, haya kweli usiyajue?
Upofu usiulee, shimoni utumbukie,
Taifa kama kijiwe, viranja wanakijiwe!
Msanja ni wako wewe, siye maswezi tutue,
Changa kalirushe wewe, kilichopo ukatoe,
Kupika umepika weye, kwanini usipakue?
Taifa kama kijiwe, viranja wanakijiwe!
Nasaba wataka wewe, na hatua kachukuwe,
Orofa kashikiliye, ya chini ising'olewe,
Abunuwasi uwe wewe, tena kwa sana ujuaye,
Taifa kama kijiwe, viranja wanakijiwe!
Kapange ukapanguwe, lakini watu si mawe,
Yatima wamfaaye, si walozaliwa naye,
Watu baki utambuwe, ndio wakuokoae,
Taifa kama kijiwe, viranja wanakijiwe!
Februari 6, 2012
Dar es Salaam.
Monday, February 6, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment