Tuesday, February 14, 2012

Uongozi sio njaa


Viongozi wenye njaa, Jethwa wakamzidia,

Yafaa kuwaambaa, msiipate balaa,

Hawa mkitunukiwa, nchi mtaikimbia,

Uongozi sio njaa, uongozi njaa baa!

Rahisi kununuliwa, vibaya ukatumiwa,

Wakabaki kuumia, raia bila hatia,

Na nchi ilivyokuwa, ni vigumu kuwatoa,

Uongozi sio njaa, bali uongozi njia!

Tajiri wasio njaa, nadra kuwachagua,

Wengi ni wenye tamaa, kutaka kujiongezea,

Hawatosheki tambua, hadi mwisho wa dunia,

Uongozi sio njaa, uongozi njaa baa!

Fukra weza jaliwa, hali waliyoridhia,

Ikawa wapigania, wa chini kuwanyanyua,

Kwa imani kuwakaa, na utu ukawajaa,

Uongozi sio njaa, bali uongozi njia!

Nadra kuwang'amua, juu hawatatokea,

Chini huwa wajichmbia, uchu kwao ni kinaya,

Yabidi kuwaibua, juu wakatokezeya,

Uongozi sio njaa, uongozi njaa baa!

Nchi inayojijua, hili huliangalia,

Muda itauchukua, kila kitu kupimia,

Na ikishawagundua, nchi wanakabidhiwa,

Uongozi sio njaa, bali uongozi njia!

Si watu wa kuongea, kazi zao huazimia,

Kila wanalofikiria, ni la wote kuwafaa,

Ubinafsi huambaa, na za kijinga tamaa,

Uongozi sio njaa, uongozi njaa baa!

Uchamungu hujaliwa, kama Omari kwa tabia,

Kutwa huwa wanalia, watu kuwahudumia,

Sio kujitafutia, kwa isoisha njaa,

Uongozi sio njaa, bali uongozi njia!

Kuna shehe huugua, na padri kufulia,

Hili kutolifikia, shetani huwazuzua,

Unafiki hujitia, wafuasi wakavia,

Uongozi sio njaa, uongozi njaa baa!

Tusomjua hutokea, mamlaka kuchukua,

Tukamuona hidaya, nchi kuiangalia,

Wagumu kujipatia, bila Mola kumrudia,

Uongozi sio njaa, bali uongozi njia!

Watu wote hujaliwa, kama yao majaliwa,

Watu wanaowafaa, wachamungu hujaliwa,

Wachamungu walokuwa, na baraka wakapewa,

Uongozi sio njaa, uongozi njaa baa!

Waovu watajaliwa, waovu waliokuwa,

Laana kuwaandamia, nuksi nazo balaa,

Hekima kuwaambaa, kitanzi wakajitia,

Uongozi sio njaa, uongozi njaa baa!

No comments: